KIKULACHO KIKO AKILINI MWAKO!!

Posted on

Watu wengi ukiwauliza ya kwamba mtu anapo umwa na nyoka ni nini kinacho muua mtu yule? Jamaa watakujibu ya kwamba Sumu kali ya nyoka ndiyo inayo muangamiza mtu huyo. Madaktari katika vituo vya matibabu pia watakupatia jibu sawa na hilo….mitaa ya akilini mwangu, wahenga watakuambia kuwa, sio sumu inayompatia mtu huyo hasara kubwa bali hasara kubwa hutokana na uamuzi wake kwa uoga na hamaki, anapo amua kumfukuza nyoka yule pindi anapo umwa. Hatua hiyo ndiyo inayompatia madhara makubwa jamaa yetu kwa sabau ndiyo inayo kimbiza damu kwa kasi mno hadi ndani ya roho na kisha kwenye ubongo na hatimaye kumpiga na chini mtu huyo. Lau jamaa anapo umwa na nyoka na aamue kuwa tukio hilo lishatendeka na cha muhimu ni kutulia, na kukaza mguu ili damu isiende kwa kasi mwilini na kutembeza sumu, basi jamaa yetu huenda akawa na nafasi kubwa ya kupona tukio hilo!

Ni kweli kabisa ya kwamba mazingara na mazingira yetu yako na sehemu kubwa katika kutujenga sisi ki mawazo na pia ki fikra. Mara nyingi tabia na mienendo ya mtu hutegemea pa kubwa mazingira na mazingara ambayo mtu huyo amekulia. Wengi wetu tuko na hadithi nyingi zinazo husiana na maisha yetu tulio yapitia na tuliyo yaona ambapo mara nyingi tunayahusisha mapito yetu kana kwamba ndiyo yalitugeuza tukawa jinsi tulivyo. Mwingine utasikia akisema kwamba yeye hakuwa na baba mlezi maishani mwake na ndiyo sababu hana nidhamu au hakuna mtu atamuambia lolote, mwingine naye atasema hawezi kupenda tena maana wanaume wote ni mafisi baada ya uhusiano wake kuenda mrama, mwingine atasema hapendi wanawake sababu alitendewa mabaya flani hapo awali, na kadhalika.

Tunapo patikana na jambo flani huwa tunakimbia kutafuta singizio la jambo lile kututendekea na kujiondolea lawama kisha tunaridhika. Hii huwa kwa sana haswa mtu anapo jua ya kwamba anaishi na virusi vya ukimwi. Wanawake kwa sana watasema ni mume ndiye aliyempatia kwa kuenda kwa malaya. Hii huwa noma sana maana katika ndoa hata kama siye mume aliye leta virusi hivyo ndani ya nyumba, watoto mara nyingi wataamini kuwa baba yao ndiye mhalifu na hawatakuwa na uhusiano mwema naye kama mama yao. Majamaa huzidiwa na mawazo na kufariki mapema. Mimi najua kuwa virusi vya H.I.V havisababishwi na wake au waume bali vinasababishwa na vijidudu flani hatari!!!

Acha nikupe mfano wangu niliyo upitia. Wakati mmoja nilikosa kazi na nilikuwa katika hali ya ufukara kabisa. Mwili ulikuwa umebaki “frame” ndugu yangu, ilhali hapo awali, nilikuwa mtu mnene mcheshi mwenye kupenda raha na furaha sana, nilikuwa wa haraka kutoa mawaidha kwa wenzangu mitaani na pia sikuwa mchoyo katika kuburudisha marafiki, nilikuwa rappa wa kukubalika katika kikundi cha UKOOFLANI. Maisha yalinigeukia na nikajipata peke yangu!
Baada ya kuhangaika nikizunguka Kenya yetu hii nikijaribu cha kufanya, nilishindwa kabisa. Nilikuwa kama vile nanuka mavi maana kila mtu niliye mwendea kutafuta msaada, aliishia kunifukuza kwake, awe jamaa au rafiki.

Nilienda sehemu nilipokuwa nikifanya kazi kama mwalimu wa ziada ili kujaribu nafasi yangu tena, maana nilijua watanikubali kwa kunifahamu na kuitambua kazi yangu…Nilipata mshangao nilipofika hapo na jamaa mmoja alipo niona nilivyo dhohofika kimwili, akaanza kucheka na kumuuliza jamaa kando yake…….”ushaona mtu anakufa ukafurahi sana japo hamna lolote utakalo rithi kutoka kwake???…… Mwenzangu, nilijionea mchawi live!! Sikudanganyi rafiki yangu kuna watu wana bahati sana walizaliwa mijini maana roho zao zina ashiria kana kwamba wangezaliwa na kuishi vijijini, wange waroga watu sana! Niliumwa na roho sana sikudanganyi. Nilikosa pa kuenda na nilishindwa la kufanya lakini Mungu sio athumani nilijipata katika kitingoji duni cha MBURUKENGE nilipo enda kuanzia maisha.

Watu wengi huwa ni rahisi kupoteza njia kabisa wanapo jikuta katika hali hiyo na pia wagundue ya kwamba wanaishi na virusi vya UKIMWI. Wengi hukubali sumu hizo za kutoka vinywani mwa watu ziwaingie akilini na kuwapatia mawazo na presha za kuishia kujinyonga au kulewa kupindukia hadi kukanyagwa na magari. Mimi baada ya tukio hilo nilibadilika sana.. Huyo jamaa aliye taamka maneno hayo ndiye aliye wakisha moto wangu wa kutetea haki za waathirika wenye kuishi na virusi vya H.I.V, ambao umenipelekea kufanya mengi kunzia siku hiyo hadi leo hii ninapo andika habari hii.

Usikubali sumu ya maneno ikufikiye ndugu yangu. Sumu kali kwanza na hatari ni inayotoka kwa wale watu unao wapenda sana na unaowajua kama jamaa zako wa karibu mno. Tangu siku hiyo mimi niliamua sitishiki, na wala sibabaishwi na sumu za midomo ya watu…Ni wazi kuwa kikulacho ki nguoni mwako, lakini cha nguoni hakina hatari sana kuliko cha kwenye akili. Jambo baya maishani ni kujihukumu mwenyewe. Sasa ukijihukumu mwenyewe wakili ni wa kazi gani? Mimi nilipata motisha kabisa kutokana na matamshi ya jamaa huyo na ndiyo yalinipatia nguvu kabisa japo yeye alifahamu kuwa ndiyo ulikuwa msumari wa mwisho wa kwenye jeneza.